LOUIS Van Gaal atawaomba wachezaji wake kumpa zawadi ya kuondokea siku ya jumamosi ili awe kocha wa kwanza wa Uholanzi kushiriki kombe la dunia bila kufungwa.
Kocha huyo wa Uholanzi atajiuzulu ili kujiunga na klabu yake ya Manchester United mara baada ya kumalizika kwa mechi ya mshindi wa tatu kesho dhidi ya wenyeji Brazil, mjini Brasilia.
Uholanzi walipoteza mechi ya nusu fainali dhidi ya Argentina kwa mikwaju ya penati siku ya jumatano-lakini Van Gaal ana hamu ya kuhakikisha timu yake inashinda ili kuweka rekodi ya timu hiyo kuondoka kombe la dunia ikiwa imefungwa kwa penati tu.
“Itakuwa sehemu ya hotuba yangu nitakayotoa kwa mara ya mwisho na naamini wachezaji wanataka kunipa zawadi kwa njia ya ushindi ili tubaki kuwa timu ambayo haijafungwa,” Van Gaal amewaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa kabla ya mechi leo ijumaa.
“Polepole, lakini kwa uhakika tunajua kuwa tunatakiwa kushinda. Timu ya Uholanzi haijawahi kurudi nyumbani bila kufungwa, sasa ndio nia yetu kwa sasa”.
“Kuna kitu tunatakiwa kufanya. Bado tunaweza kuweka rekodi kwasababu Uholanzi ilipoteza mechi mwaka 1974 na 1978”.
Van Gaal ameumia kucheza mechi ya mshindi wa tatu baada ya kupoteza kwa penati dhidi ya Argentina na amekiri Uholanzi inaendelea kuimarika baada ya kushindwa kufika fainali.
“Ilikuwa huzuni kubwa sana, sana, sana na ndoto ziliyeyuka. Haitaweza kurudia tena, lakini lengo lilikuwa ni kuwa wa kwanza”. Aliongeza Van Gaal.
Post a Comment